Mungu Ana Matarajio Gani Kwangu?
Sikiliza makala hii:
Kama wewe ni kama Wakristo wale wengine basi ndani mwako kuna shauku la kumpendeza Mungu kupitia kwa maisha yako. Lakini kusema kweli, wakati mwingine wewe unajihisi kuchoka kwa kufanya bidii zote za kuishi maisha ya Kikristo. Hata wakati mwingine wewe hujihisi kugandamizwa sana na swala hili.
Wakati nilipokuwa kafiri dhambi haikuwa jambo ambalo nilitilia maanani sana. Kusema kweli mimi sikulifahamu jambo hilo vizuri. Na ndiposa sikujihisi kuhukumiwa. Lakini nilipofanyika kuwa Mkristo . . . papo hapo jambo hilo likaingia ndani yangu! Nikajipata kwamba kuna mambo ambayo nilikuwa nafanya ambayo sasa Mungu hakuyataka maishani mwangu. Nikaanza kutambua haja ya kuwapenda watu wale wengine, kusoma biblia, kuomba, kushuhudia, kuwafunza Wakristo wenzangu, n.k. Ndiposa nyakati zingine nikawa na mawazo kwamba, “Kumbe kuwa kafiri lilikuwa ni jambo rahisi hivyo.” Kwa sababu sasa nilikuwa nimemjua Mungu, nilijihisi mtu mwenye jukumu kubwa la kumpendeza Mungu maishani mwangu. Basi nikawa nasoma Biblia, nasoma amri moja ya Mungu au nyingine, na kila mstari wa Biblia ukawa waniletea fikira kwamba, “Hili ni wazo nzuri. Mimi nahitaji kufanya mambo mengi zaidi kama haya.”
Lakini mimi nilisaidika wakati Mungu alinifundisha ukweli fulani katika Biblia ambao uliniweka huru kabisa mpaka nikaweza kuachana na mwelekeo huo wa kuona kwamba nilihitaji kufaulu katika majukumu na matendo, na hapo ndipo nikaweza kumwona Mungu tena, na kupata tena kufurahia uhusiano kati yake na mimi. Kanuni hii ambayo niliitambua ni ile ambayo kwa kweli inapatikana kote katika Maandiko, katika vitabu vya Warumi, Wagalatia, Waefeso, Wakorintho wa Kwanza na hata wa Pili . . . kusema kweli hili ni jambo linalopatikana kote katika Agano Jipya.
Ukweli wenyewe ni kwamba: Mungu hana tarajio kwamba sisi tutakuwa wakamilifu. Mungu hatarajii kwamba tutafikia viwango fulani vya ukamilifu maishani mwetu. Mungu kamwe hadhani kwamba sisi tunaweza kuishi maisha mema ya Kikristo, na kwa kweli Yeye hatarajii kwamba tunaweza kufikia viwango vya utakatifu anavyotaka. Kama kweli Yeye angalidhani hivyo, basi Yesu hangefika ulimwenguni na kufa kwa ajili yetu. Lakini kwa kweli hayo ndio ambao Yesu alifanya.
Yesu aliambia umati kwamba, “Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” Kwa hivyo ni kweli kwamba sheria zake Mungu na amri zake zinadai kwamba tuwe wakamilifu. Lakini kama Mungu angetukubali kulingana na vile ambavyo tunaishi maishani mwetu, kwa kulingana na amri zake, basi ingemaanisha kwamba sote ni lazima tungekuwa wakamilifu. Lakini Yesu alikuja ili kutuokoa kutokana na adhabu ya dhambi zetu!
Mungu anajua pengo lililoko kati ya ukamilifu wetu ikilinganishwa na hali yetu ya dhambi. Hata wakati tumefanyika kuwa Wakristo, kungali kuna mvutano mkubwa ndani yetu unaotokana na juhudi zetu za kuziba pengo hilo, ili kwamba tuweze kujihisi starehe za kuwa karibu na Mungu. Wengine wetu hujaribu kuziba pengo hilo kwa kudhalilisha viwango vya utakatifu ambavyo Mungu ametuwekea kama Wakristo: “Kusema kweli Mungu hakumaanisha hivyo.” Ilhali wengine wetu hujaribu kuziba pengo hilo kwa kufanya bidii zaidi katika matendo yetu: “Nitajitahidi zaidi . . .”
Lakini Mungu anasema nini kuhusu pengo hili? Yeye anasema kwamba pengo hilo liko, na daima litakuwako. Lakini sisi ambao tumeweka imani yetu kwa Yesu na kumpokea maishani mwetu, tayari tumesamehewa, na tumetangazwa kuwa wenye haki, walio wa thamani kubwa machoni pake, na kwamba Yeye ametushika na kutuongoza kwa mkono wake ambao hututunza. Sisi ni wake kabisa na anatupenda bila pingamizi au vizuizi vyovyote vile, hata wakati ambapo pengo lingali lipo.
“Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa waadilifu kupitia kwa imani, basi tunayo amani naye Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la kushiriki utukufu wa Mungu” (Warumi 5:1,2).
Lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba tutafika mahali maishani mwetu ya Ukristo ambapo tutakuwa na mawazo kwamba Mungu ataka tulipe wema wake kwa njia moja au nyingine.
Ndiposa lengo la makala haya ni kukusaidia wewe ili usianguke katika mtego huo wa kuhisi kwamba ni lazima ufaulu katika matendo fulani ili upate kumpendeza Mungu. Maandiko yanatuonya dhidi ya mawazo kama hayo, kwa sababu mawazo hayo hutunyang’anya furaha yetu ya kumjua Kristo.
Basi hebu tutazame kwa makini yale ambayo Mungu amesema kuhusu uhusiano wetu na Yeye. Hebu tutazame miongozo ambayo tayari ishaandikwa, na ambayo Mungu mwenyewe ameyasema kuwa ni ya kweli kuhusu uhusiano wako na Yeye.
Vile Ambavyo Wewe Ulifanyika Kuwa Mkristo
Hebu tazama (hapa chini) majukumu ambayo Mungu alibeba ili wewe ufanyike Mkristo ikilinganishwa na jitihada zako.
- Mungu alikuchagua wewe kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu na kukuita ili uwe wake (Waefeso 1:2; 2 Timotheo 1:9).
- Mungu alikuja ulimwenguni kwa ajili yako (Yohana 3:16).
- Kibinafsi Mungu alikufa kwa ajili yako (Warumi 5:8).
- Mungu alihakikisha kwamba kutakuwako na mtu wa kukwambia kuhusu Injili (Waefeso 1:13).
- Mungu alijitoa na kuingia maishani mwako (Ufunuo 3:20; Yohana 1:12,13).
- Mungu alikupatia shauku yla kumjua na la kuitikia wito wake (Ufunuo 3:20).
- NI wakati huo wewe ulimgeukia na kumpokea.
- Mungu naye akaingia maishani mwako na akakutangaza kuwa mwenye haki, ambaye tayari ashasamehewa, na kukuita ili uwe wake (1 Yohana 3:1; Wakolosai 1:13,14; Waefeso 1:4; Yohana 1:12).
Wewe ukafanyika kuwa Mkristo kwa tendo rahisi la kumwitika Mungu kwa imani. Vivyo hivyo ndivyo Yeye anataka uishi maisha yako ya Ukristo . . . kwa kumwitika Mungu kwa imani. Ugumu na uwezo wa kutimiza hayo yote uko mikononi mwa Mungu. Lakini sasa wewe huenda unafikiria kwamba, “Jambo hili ni rahisi sana. Sioni cha ukubwa hapa?” Shida ni kwamba, karibu kila Mkristo hujipata amejikwaa katika jambo hili kwa wakati mmoja au mwingine. Kwa nini?
Ni tabia ya kibinadamu mtu kufikiria kwamba ana deni la Mungu kutokana na yale ambayo Mungu amemfanyia. Pili, ni asili ya wanadamu kufikiria kwamba kwa sababu mtu sasa amejua mambo kadhaa kutoka kwa Biblia, eti kwa sababu sasa amejua mambo machache kuhusu maombi, au kwa sababu sasa anaelewa kidogo kuhusu kuwashuhudia watu kuhusu Mungu . . . sasa basi atachukua jukumu la kuwa “Mkristo mzuri.” Ukweli ni kwamba, jambo hilo litakunyang’anya furaha yote ambayo unastahili kuwa nayo kutokana na kumjua Mungu.
Na kama kibinafsi wewe hufanyi uamuzi huo kwamba unahitaji kutimiza matakwa fulani ili Mungu akupende, Wakristo wenzako hufana sana katika jitihada za kumfanya mtu kujihisi kuhukumiwa, na kujihisi kusukumwa na matarajio kwamba anahitaji kumtii Mungu zaidi. Ni tumaini langu kwamba makala haya yatakuwezesha kuelewa kutokana na Maandiko, vile ambavyo unastahili kuishi maisha ya Kikristo bila kubeba uzito wa matarajio ambayo hayafai; eti ya kwamba unahitaji kufanya mambo fulani ili kumpendeza Mungu, na kutimiza matakwa yake. Makala yenyewe yatakuonyesha vile ambavyo Mungu anakupenda, na pia vile ambavyo Yeye anataka uwe na uhusiano na Yeye.
Kusema kweli Mungu hakuanzisha uhusiano wako na Yeye ambao ulikutegemea wewe, bali uhusiano huu daima humtegemea Mungu. Hebu nifafanue jambo hili kwa kutumia Maandiko yafuatayo:
Sisi Hukubalikaje na Mungu?
Wewe ulitangazwa kwamba umesamehewa dhambi zako kwa sababu ya neema (fadhili) zake Mungu, kutokana na kifo ambacho Yesu alikufa kwa sababu yako. Si ni ukweli kwamba wewe ulipokea kipawa cha msamaha wako kutokana na kuamini kwamba Yesu alilipa gharama ya dhambi zako? Kusema kweli wewe hukufanyia kazi msamaha huo. Jukumu lako lilikuwa kumwamini Mungu tu wakati Yeye alisema kwamba amekusamehe.
“. . . wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake . . .” (Tito 3:3-7). “Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo! . . .” (Waefeso 1:7).
Je, kwa sababu sasa wewe ni Mkristo ukweli huo sasa umebadilika? Je, Mungu sasa ana ratiba ndefu ya mambo ambayo anatarajia ufanye? La, hasha. Lakini sasa wewe tayari umeanza kufikiri kwamba, “Subiri kidogo. Si Biblia IMEJAA amri nyingi? Huwezi kamwe kusoma hata aya moja bila kuambiwa kila ambacho unastahili kufanya.” Hiyo ni kweli kabisa. Lakini hata ingawa Mungu amekupatia amri zake, Yeye pia amekuambia kwamba huwezi kutii amri hizo kwa njia kamilifu. Hata amesema kwamba wakati ambapo unajikaza kisabuni huku ukijaribu kutii amri hizo ndivyo ambavyo utagundua kwamba dhambi zako ni nyingi mno (Warumi 3:20). Zaidi ya hayo, kwa kiwango kile ambacho utafanya bidii katika jambo hilo, ndivyo ambavyo utajisikia kwamba umekosea, ya kwamba wewe ni mtu ambaye unastahili hukumu na adhabu yake Mungu, maanake utajisikia uko mbali sana na Mungu.
Hata mtume Paulo alizungumza kuhusu hisia zake za kukata tamaa ambazo zilimwandama. Yeye alitazama sheria ya Mungu na kusema kwamba, “Amri ni takatifu, ya haki na nzuri.” Lakini kwa kiwango kile ambacho alijaribu kufuata amri hizo ndivyo ambavyo aliendelea kutenda dhambi. Ndiposa akasema, “Ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza . . . nafanya lile baya nisilotaka” (Warumi 7:18-19). Basi kwa kukata tamaa kabisa yeye akasema kwamba, “Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka mwili huu unaonipeleka kifoni?” Na suluhisho lake lilikuwa kwamba, “Shukrani kwa Mungu afanyaye hivyo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo!” (Warumi 7:24-25).
Tunahitaji kukabili hisia zetu zinazotwambia kwamba tumeanguka, kwamba tumetenda dhambi, na zinazofanya tuhisi kuhukumiwa kwa kutumia Maandiko. “Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo” (Warumi 8:1). “Maana, tulipokuwa bado maadui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uhai wa Kristo” (Warumi 5:8-10).
Basi unapotafakari amri zake Mungu, wewe usijaribu kuzitii kwa juhudi zako mwenyewe . . . badala yake mwombe Mungu, ambaye anaishi ndani yako, ili aunde uwezo huo ndani yako. Kama Mungu amesema tupendane, lengo lake si kwamba tufanye bidii na kuchukua jukumu la kumwonyesha vile ambavyo tumejaa upendo ndani yetu. Badala yake Yeye anataka tumtegemee na kumwambia, “Mungu ninakuomba uishi ndani ya moyo wangu ili niweze kumwona mtu huyu kama ambavyo unamuona, na uweke ndani yangu upendo kwa ajili yake kama vile ambavyo wewe unampenda. Mimi kamwe siwezi kumpenda kwa juhudu zangu mwenyewe, lakini naomba kwamba upendo wako mkuu uundike ndani yangu kwa ajili yake.”
Tofauti ni nini?
Tofauti yake inahusu mtu kufanya bidii ya kibinafsi ili kumpendeza Mungu, ikilinganishwa na mtu kumtegemea Mungu ili Mungu mwenyewe aweze kuishi maisha yake ndani yako. Kusema kweli sisi kamwe hatutawahi kukomaa na kufikia mahali ambapo tutakuwa huru kuishi bila Mungu. Badala yake sisi hukomaa kwa kumtegemea Mungu, na shauku lake ni kwamba tufanye hivyo. Yeye anataka tufurahie uhuru na upendo wa kuwa na uhusiano na Yeye; huku tukimwamini na kumtegemea. Yeye kamwe hana tarajio kwamba kwa juhudi zetu wenyewe na kwa kuhitimu kwetu tunaweza kufanya mambo ambayo yanampendeza.
Biblia inaita amri za Mungu “Sheria.” Kwa sababu wewe sasa ni Mkristo hauko tena chini ya himaya ya sheria au chini ya hukumu na adhabu ya Mungu – badala yake wewe umesamehewa na una uzima wa milele. Umewekwa huru kutokana na matakwa ya sheria.
Mtume Paulo alisema kwamba, “Lakini, tunajua kwa hakika kwamba mtu hawezi kufanywa mwadilifu kwa kuitii sheria, bali tu kwa kumwamini Yesu Kristo. Na sisi pia tumemwamini Yesu Kristo ili tupate kufanywa waadilifu kwa njia ya imani yetu kwa Kristo, na si kwa kuitii sheria” (Wagalatia 2:16).
Je, mtume Paulo alitilia mkazo amri za Mungu kwa kiwango kipi, na alifanya jitihada gani ili kuzitimiza amri hizo? “Maana, kuhusu sheria hiyo, mimi nimekufa . . . nipate kuishi kwa ajili ya Mungu. Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani . . . Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu. Sipendi kuikataa neema ya Mungu. Kama mtu hufanywa mwadilifu kwa njia ya sheria, basi, Kristo alikufa bure!” (Wagalatia 2:19-21).
Kabla ya kumpokea Yesu wewe ulikuwa mbali na Mungu, ulikuwa tu na uwezo wa kujua amri zake, na hukumu yake ilikuwa juu yako. Lakini sasa tayari ushamjua Kristo, na Roho wake anaishi ndani yako.
Mungu anasema, “Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao.” Na mahali papo hapo anaendelea kusema, “Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu” (Waebrania 10:16,17). Kwa hivyo, badala ya sheria kuwa juu yako, na kukusumbua kwa ajili ya matakwa yake, Mungu ameweka sheria yake moyoni mwako, na kulingana na vile ambavyo Roho Mtakatifu atakavyokubadilisha, Yeye ataendelea kuzidishia shauku ndani yako ya kufanya mambo yale ambayo yanampendeza Mungu. Na kulingana na vile muda utavyoendelea kuyoyoma, na wewe kuendelea katika uhusiano wako na Yeye, Mungu ataendelea kukuza ndani yako shauku na uwezo wa kuishi maisha matakatifu mbele zake.
“Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu” (Waefeso 2:8,9).
Mungu ana mpango kwa ajili ya maisha yako, na mpango wenyewe ni wa kutumia maisha yako ili yawe baraka kwa watu wale wengine, na kwa ajili ya utukufu wake. Sasa wewe tayari una uhusiano na Mungu, na ni Yeye ambaye anaishi maisha yake ndani yako, na pia kuendeleza kazi njema ndani yako.
Lakini tutashughulikia dhambi kwa njia gani?
Lakini hebu sasa niulize swali: Tuseme umemwomba Mungu aunde tabia fulani maishani mwako, au kwamba akuweke huru kutokana na tabia fulani, lakini ujipate kwamba unaendelea kushindana na jambo hilo maishani mwako. Je, utafanya nini ukijipata kwamba hasira yako ingali inakwandama, au kwamba ungali unaanguka majaribuni, au kujipata kwamba hauwi mwaminifu kwa maombi au katika kusoma Neno la Mungu kwa kiwango kile ambacho unatakiwa kuwa? Sasa utafanyaje? Je, hivi ni kusema kwamba huu ni wakati bora wa wewe kuanza kujichukulia jukumu la maisha yako ya Kikristo kwa kufanya bidii zaidi? La, hasha. Kwa nini? Kwa sababu kwa kiwango kile ambacho utajaribu kufanya mambo hivyo kwa lengo la kumfurahisha Mungu, ni kwa kiwango hicho utakosa kufuzu katika jitihada hizo zako, na wewe utaendelea kujihisi kuwa mbali na Mungu, na kukosa furaha ya kumjua Mungu.
Ni rahisi kwa Mkristo kufikiria kwamba Mungu hutulipa kulingana na bidii zetu, kwa sababu hivyo ndivyo jamii zetu hufikiria . . . kwamba tukijitwika jukumu fulani, tufanye bidii sana, tujikaze kisabuni . . . basi tutapata malipo ya bidii zetu. Mkristo anaweza kutazama amri zake Mungu ambazo zinapatikana katika Biblia na kuanza kufikiri, “Kwa kweli nikijaribu sana naweza kufaulu kufanya jambo hili.” Lakini ni wakati kama huo ambapo mtu hujipata amekata tamaa kwa sababu Biblia yenyewe inasema kwamba mtu akitilia umuhimu sheria yeye hupata matokeo moja tu . . . la kutambua kwamba yeye ni mwenye dhambi. Mungu hakuanzisha uhusiano kati yako na Yeye ili wewe ufanye bidii au ulipe malipo yake. Badala yake msingi wa uhusiano huo wetu na Yeye ni kwamba Yeye anataka sisi tumtumaini Yeye ili aweze kukuza ndani yetu kile ambacho kitampendeza kupitia kwa maisha yetu.
Wakati wewe ungali hapa duniani bila shaka utaendelea kutenda dhambi. Kamwe hutawahi kuwa mtu mkamilifu katika maisha haya. Wewe unajua ukweli huo, na hata Mungu anaujua. Basi wakati umetambua kwamba kuna dhambi maishani mwako ungama dhambi hiyo, na uamini yale ambayo Mungu amekuahidi.
“Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote” (1 Yohana 1:9).
Kuwa na subira wakati unapomruhusu Mungu kukubadilisha
Weka umuhimu kwa swala la wewe kumjua Mungu. Fanya bidii kumjua kupitia kwa maombi, kwa kusoma Biblia, na kwa kuwa na ushirika wa kujifunza Biblia na Wakristo wale wengine . . . yote hayo yanafaa. Lakini imani yako isiwe katika bidii zako, lakini iwe katika uwezo wa Mungu wa kufanya kazi yake maishani mwako. Yesu alifananisha jambo hili na zabibu zinazopatikana katika mti wa mzabibu. Akasema kwamba Yeye ni kama mti wa mzabibu, na sisi ni kama matawi ya mzabibu huo. “Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Kama vile tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipobaki katika mzabibu, hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu” (Yohana 15:4).
Akaendelea kusema, “Mimi nimewapenda nyinyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu” (Yohana 15:9).
Lakini si ni kweli kwamba Yesu alitwambia “mtii amri zangu”?
Njia ambayo inafaa wewe kuishi, na ambayo itakuwezesha kuwa na uhai tele ambao Yesu alizungumza kuhusu, na pia kukuwezesha kuwa na uhakika na upendo wake kwako, ni kwa wewe kufanya kile ambacho amekwambia ufanye. Yeye akasema kwamba, “Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike” (Yohana 15:10,11). Yeye anataka sisi tuishi kulingana kwa njia ambayo Yeye mwenyewe alisema kwamba itatuwezesha kufurahia upendo wake, na tuwe na furaha katika maisha yetu ya Ukristo. Lakini njia ya pekee ambayo kupitia kwake tutaweza kutii amri zake ni kwa kumtegemea Yeye wakati ambapo tunafuata amri hizo.
Basi wakati wowote ambapo mimi napatana na mstari wa Biblia ambao Mungu amesema, “Fanya hivi . . .”, mara moja mimi humwambia Mungu yafuatayo, “Hili ni wazo bora kabisa. Mimi ningependa maisha yangu yakupendeze, na naomba wewe ufanye jambo hili kukua maishani mwangu kupitia kwa Roho wako. Nipe uwezo wa kutii jambo hili. Kwa kweli mimi nikijaribu kufanya hili kwa uwezo wangu mwenyewe bila shaka nitaambulia patupu. Lakini naomba kwamba ubadilishe mawazo yangu au ufanye ndani yangu kile ambacho unataka kufanya ili maisha yangu yaweze kuambatana na andiko hili.” Na kutoka hapo mimi huwa sisumbuliwi tena na swala hilo. Huenda pengine niandike mstari huo mahali fulani, ili niweze kuwaza juu yake, au hata niweze kuukariri. Lakini imani yangu ya kufaulu kutii andiko hilo huwa katika Mungu.
Yesu ametuweka huru kutokana na matakwa ya sheria, na anakukaribisha tupate pumziko lake, basi tumtegemee Yeye . . . na tuweze kudumu mahali ambapo tunaweza kufurahia uhusiano wetu wa karibu pamoja na Yeye.
“Hali kadhalika nyinyi ndugu zangu: nyinyi pia mmekufa kuhusu sheria kwa kuwa nyinyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka kwa wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu” (Warumi 7:4).
“Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya sheria . . .Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho . . .” (Warumi 7:6).
“Maana kwa kuja kwake Kristo, sheria imefikia kikomo chake, ili wote wanaoamini wafanywe waadilifu” (Warumi 10:4).
“Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu . . .” (Warumi 4:5).