Siri ya Mkristo
Kuelewa maisha ambayo yamejazwa Roho Mtakatifu.
Sikiliza makala hii:
Je, kuishi maisha ya Kikristo kunaonekana kuwa ni jambo ambalo haliwezekani? Basi hebu nikwambie siri—kwa kweli hilo ni jambo lisilowezekana—tukiwa peke yetu. Kuishi maisha ya Kikristo kwa kutumia nguvu zetu wenyewe ni kama kujaribu kuendesha meli katika nchi kavu . . . kwa kweli mtu hawezi kufaulu. Ili meli iende mahali popote pale inahitaji kuwa imetua juu ya maji. Na ili mtu aweze kufurahia maisha yake ya Kikristo anahitaji kujifunza kuwa na pumziko ndani yake Mungu. Mtume Paulo alifahamu jambo hilo vizuri: “Naweza kuikabili kila hali kwani Kristo hunipa nguvu” (Wafilipi 4:13).
Siri ya Mkristo ya kuweza kuishi maisha yenye ushindi ni kwa kumruhu Kristo kuishi maisha yake Mwenyewe ndani yetu: “Mimi nimeuawa pamoja na Kristo msalabani, na sasa naishi, lakini si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu. Maisha haya ninayoishi sasa naishi kwa imani, imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili yangu” (Wagalatia 2:20).
Jioni ile, siku ya mwisho ambayo Kristo alikuwa na wanafunzi wake, ndipo aliwaambia kwamba Yeye angewaacha, lakini kamwe hawangebaki peke yao: “Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu” (Yohana 16:7).
Basi wewe umepewa mtu wa kukwezesha kuishi maisha ya Kikristo kwa ushupavu—ambaye ni Roho Mtakatifu. Lakini Yeye sio kiongozi wa kukupatia tu habari za njia ambayo unahitaji kupitia ili ufike mbinguni: Yeye ni Roho wa Kristo—ambaye amekuja ili aishi ndani yetu.
Roho Mtakatifu ni Nani?
Roho Mtakatifu ni Mungu, kama ambavyo Mwana na Baba ni Mungu. Watu huchanganyikiwa sana kumhusu Roho Mtakatifu wanapokosa kumchukulia kama “mtu”. Yeye ana nafsi yake. Yeye ni “mtu” wa Kiungu ambaye ana hiari na hisia zake mwenyewe.
Roho Mtakatifu ana sifa ambazo Mwana na Baba wako nazo. Nguvu zake Roho Mtakatifu hazipimiki, anajua mambo yote, habadiliki kamwe, na Yeye ni wa milele. Yeye ndiye sehemu ya tatu ya Utatu wa Mungu.
Kusudi la sisi kupewa Roho Mtakatifu ni nini?
Roho Mtakatifu ni sehemu kubwa ya maisha yako ya Kikristo. Hebu tutazame baadhi za wajibu zake ili tuweze kujua umuhimu wake.
Roho Mtakatifu ndiye alikuhakikishia dhambi yako na haja yako ya kumpokea Kristo (Yohana 16:8-11). Biblia inasema kwamba bila msaada wa Roho Mtakatifu watu hudhani kwamba Ukristo ni upuzi (1 Wakorintho 1:18). Wale waliokuzunguka wanaweza kudhani kwamba wewe una akili pungufu kwa sababu ya vile umejitoa kwa Kristo! Lakini wewe kamwe huoni jambo hilo hivyo, kwa sababu Roho Mtakatifu amefungua macho yako kuona urembo wa maisha ndani yake Kristo.
Roho Mtakatifu ndiye alikupatia maisha mapya. Yesu alisema kwamba mwili huzaa mwili. Roho Mtakatifu ndiye huzaa maisha ya kiroho (Yohana 3:6). Na ni kwa kupitia Roho Mtakatifu ndipo Mungu alimwaga upendo wake mioyoni mwetu (Warumi 5:5). Pia Roho Mtakatifu ndiye hutupatia hakikisho la ndani kwamba sasa sisi ni Wakristo (Warumi 8:16).
Roho Mtakatifu ndiye mwalimu wako. Yeye hukuongoza kuweza kuelewa ukweli wa Neno lake Mungu. Yeye hukupatia maelezo ya Biblia ili uweze kuelewa na kutumia ukweli wake (Yohana 16:13,14). Yeye hunena na mioyo ya watu unapowaambia kuhusu Yesu (Matendo 1:8). Yeye ndiye hunena mbele zake Baba wakati hujui cha kusema au jinsi ya kuomba (Warumi 8:26,27).
Kristo alitutumia Roho Mtakati ili kutwezesha kuishi maisha ya Kikristo! Kama ambavyo Mtume Paulo aliandika na kusema, “. . . Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu” (Warumi 8:11). Mtu anaweza tu kuishi maisha ya Kikristo kwa nguvu zake Roho Mtakatifu.
Pengine wewe sasa unafikiri, mimi kwa kweli nahitaji Roho Mtakatifu aingie ndani yangu! Lakini ikiwa wewe ni Mkristo Yeye tayari anaishi ndani mwako: “Lakini nyinyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu” (Warumi 8:9). Roho Mtakatifu anaishi ndani yako, lakini pengine wewe hujasalimishi maisha yako kwa uongozi wake. Yeye anaweza kuwa ndani yako—bila Yeye kuwa kiongozi wa maisha yako, raisi wa kukuongoza.
Mtume Paulo alitambua Ukristo wa aina mbili: Ukristo wa kiroho na Ukristo wa kimwili.
1. Mkristo wa Kiroho: Huyu ni Mkristo ambaye anamtumaini Mungu, anayejaribu kuishi maisha yake kulingana na matakwa ya Mungu, huku akiwa na “akili za Kristo” (1 Wakorintho 2:16).
Mkristo wa kiroho amempokea Kristo na anaishi maisha ambayo Kristo Mwenyewe anaishi ndani yake. Hatusemi kwamba mtu kama huyo hatendi dhambi, na kwa kweli yeye hukutana na shida na majaribu ya kila siku kama sisi wengine. Lakini katika maisha yake yote yeye humtumaini Kristo kwa kila jambo na katika shida ambazo anakutana nazo maishani. Shauku lake kuu ni kumpendeza Kristo, na yeye hategemei kupata sifa kutoka kwa mtu mwingine yule.
2. Mkristo wa Kimwili: Huyu ni Mkristo ambaye anaishi kwa bidii zake mwenyewe na kulingana na mawazo yake. “Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo. Ilinibidi kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari kukipokea. Hata sasa hamko tayari. Maana bado nyinyi ni watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na ugomvi kati yenu? Mambo hayo yanaonesha wazi kwamba nyinyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi mtindo wa kidunia” (1 Wakorintho 3:1-3).
Tukisema “mtu wa kimwili” ni kumaanisha mtu kama huyo “anaongozwa na mwili.” Mkristo wa kimwili ni Mkristo ambaye (wakati mmoja yeye alitoa maisha yake kwa Yesu Kristo), lakini maisha yake huongozwa na maslahi yake binafsi na pia mahitaji yake. Maishani mwake kunaweza kuwa na ushahidi kwamba yeye ni Mkristo, lakini kazi ya Roho Mtakatifu maishani mwake huwa imegandamizwa, aidha kwa njia ya yeye kufanya dhambi kwa hiari, au kwa yeye kutotambua huduma ya Roho Mtakatifu maishani mwake.
Ni jambo gani hutenganisha Mkristo wa kimwili na Mkristo wa kiroho? Sio kwamba Mkristo wa kimwili amepungukiwa na Kristo au na Roho Mtakatifu—kwa kweli chanzo cha yeye kupata mambo hayo ni mahali pale tu ambapo Mkristo wa kiroho huyapata. Lakini mtu wa kiroho hutegema nguvu za Kristo kuishi maisha yake ya Kikristo, ilhali mtu wa kimwili hutegemea nguvu zake mwenyewe. Lakini kujaribu kuishi maisha ya Kikristo kwa nguvu zako mwenyewe ni jambo la kipuzi kama vile kujaribu kusafiri mpaka mjini kwa kulisukuma gari lako hadi huko.
Kuongozwa na Roho Mtakatifu
Biblia inasema kuhusu haja ya sisi “kuongozwa” na Roho Mtakatifu. Hii ni kumaanisha kwamba tunahitaji kutii yale ambayo Roho Mtakatifu anasema: Yeye ndiye hutuongoza, nasi tunafuata. Jambo hilo ni rahisi hivyo. Lakini kwa kawaida sisi hatupendi kuambiwa cha kufanya—hata kama ni Mungu Mwenyewe anatwambia! Lakini maana ya kujazwa na Roho ni kumaanisha tumruhusu Roho wa Mungu na Neno la Mungu kutwambia cha kutenda.
Kila siku tuna chaguo la kufanya: Je, sisi tutamruhusu Roho Mtakatifu kutuongoza, ama tutaongozwa na kitu kingine? Je, tutaruhusu woga wetu kuhusu siku zijazo, au shauku zetu za kutaka tutakacho ziwe muhimu kuliko kumtii Kristo? Wakati wewe umejazwa Roho Mtakatifu Yeye ndiye huongoza mawazo na matendo yako. Kusema kweli huwezi kuwa umejazwa Roho halafu na uwe umejaa chuki, woga, na masumbufu ya kiakili. Hakuna nafasi ya mambo kama hayo maishani mwetu kama tumejazwa na Roho.
“Kwa hiyo, msiwe wapumbavu, bali jaribuni kujua matakwa ya Bwana. Acheni kulewa divai maana hiyo itawaangamiza, bali mjazwe Roho Mtakatifu” (Waefeso 5:17-18). Kinyume na adhari za ulevi ambazo sio za kudumu, adhari za Roho Mtakatifu ni za kudumu. Adhari hizo hazipunguki kwa ajili ya mpito wa wakati. Biblia inaita jambo hilo tunda, ambalo huzaliwa ndani yetu kutokana na kuishi maisha ambayo Kristo anishi ndani yetu: “Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi . . .” (Wagalatia 5:22,23).
Je, Ninawezaje Kujazwa na Roho Mtakatifu?
Sisi tuna uhuru wa kuchagua kama tutaongozwa na Roho Mtakatifu. Hili ni jambo la hiari, lakini silo jambo ambalo unaweza kupitishiwa tu na mtu. Watu hawawi walevi kwa kukaa karibu na chupa za pombe ambazo bado hazijafunguliwa, au kwa kufanya kazi katika duka la kuuza pombe. Kama Mkristo unaweza kuwa umezungukwa na Biblia, na pia na Wakristo wenzako, lakini uwe kwamba bado hujajazwa Roho Mtakatifu. Lakini wewe mwenyewe unaweza kujieleza shauku lako la kumfuata Roho Mtakatifu kwa njia ya maombi. Tazama hapa chini ambapo nimeandika ombi ambalo limekuwa msaada mkubwa kwangu katika suala hilo:
“Baba Mungu, ninakuhitaji. Sasa nakiri kwamba nimekuwa nikiyaongoza maisha yangu mwenyewu, na kutokana na hayo nimetenda dhambi dhidi yako. Ninakushukuru kwa sababu umenisamehe dhambi zangu kupitia kwa kifo cha Yesu msalabani, ambacho alinifia. Sasa ninamwalika Kristo tena kuchukua mamlaka yake katika jukwaa la maisha yangu. Naomba unijaze Roho Mtakatifu kama ambavyo uliamuru kwamba nijazwe, na kama ambavyo wewe uliahidi katika Neno lako kwamba utafanya hivyo ikiwa nitaomba kwa imani. Ninaomba haya katika jina la Yesu. Na kulingana na imani yangu sasa mimi ninakushukuru kwa kuongoza maisha yangu na kwa kunijaza Roho Mtakatifu.”
Kama uliomba ombi hilo huku ukiwa na shauku la kuongozwa na Roho sasa Roho Mtakatifu amekujaza—hata kama wewe hujisikii hivyo. “Na sisi tuko thabiti mbele ya Mungu kwani tuna hakika kwamba tukimwomba chochote kadiri ya matakwa yake, yeye hutusikiliza. Yeye hutusikiliza kila tunapomwomba; na kwa vile tunajua kwamba yeye hutusikiliza kila tunapomwomba, twajua pia kwamba hutupatia yote tunayomwomba” (1 Yohana 5:14,15).
Kuna watu ambao hulinganisha kujazwa na Roho Mtakatifu na ujuzi wa kidini ambao mtu hawezi kueleza vizuri. Lakini jambo hili si fumbo bali ni uamuzi kwa njia ya imani: kukubali yale ambayo Mungu amesema katika Neno lake ambalo ni shauku lake la kutaka kukujaza na Roho wake. Wewe basi usitegemee hisia zako mwenyewe.
Maswali Matatu
Huduma ya Roho Mtakatifu ni kitu muhimu sana katika maisha yetu ya Kikristo! Lakini pengine ungali na maswali kadhaa.
1. Ni kwa nini idadi kubwa zaidi ya Wakristo hawajazwi Roho Mtakatifu?
Hilo ndilo swali Mike aliniuliza siku ile tulikula chakula cha mchana pamoja. Ni kwa nini Wakristo wengi zaidi hawajazwi Roho Mtakatifu?
Jibu rahisi ni -- ni kwa sababu ya dhambi. Sisi hufanya chaguo la kutomtii Mungu. Wakati mwingi kutotii huku hujitokeza kama kiburi: kutaka kufanya mambo kwa njia yetu wenyewe. Hatutaki kumruhusu Mungu aongoze maswala yetu ya kifedha, huku tukijiambia kwamba tumesumbuka sana kupata pesa hizo, na kwa hivyo pesa hizo ni zetu wenyewe. Pia hatumruhusu Mungu kuongoza mahusiano yetu; ni kwa nini tumsamehe mtu kama huyo na ni yeye wa kulaumiwa? Hatumpatii Mungu uongozi wa maadiili yetu; hili jambo si la mtu mwingine—hata Mungu hahusiki hapa. Hapa ni kiburi kinaongea. Maandiko ya Mungu yanasema, “Yeye huwadharau wenye dharau, lakini huwafadhili wanyenyekevu” (Mithali 3:34).
Dhambi hii pia huvaa vazi lingine: vazi la woga. Mithali moja inasema, “Kuwaogopa watu ni kujitega mwenyewe” (Mithali 29:25). Je, kuna jambo ambalo Mungu angetaka ufanye lakini wewe hujafanya hivyo kwa sababu unaogopa vile watu wengine watafikiria? Najua ni rahisi mimi kufikiria hivi: kamwe siwezi fanya hivyo. Nikifanya hivyo nitaonekana mtu mpumbavu. Kwa kweli Mungu hawezi kunitaka kufanya hivyo. Lakini ukweli ni kwamba -- wakati mwingi Mungu Mwenyewe hutaka tufanye hivyo!
Sehemu ya mwisho ya aya ya Maandiko ambayo tumenukuu hapo juu inatufundisha kwamba: “Lakini anayemtumaini Mwenyezi-Mungu yu salama.” Ni rahisi mtu kuweka kibali cha mwanadamu zaidi ya kibali chake Mungu, lakini ukweli ni kwamba, ndani yetu tunachotaka zaidi ni kumpendeza Mungu. Bila shaka maisha yetu yatakuwa tofauti na ya watu wale wengine. Lakini hiyo ni gharama ambayo tunastahili kulipa.
2. Je, ninaweza kuwa nimejazwa na Roho na niwe bado nang’ang’ana na dhambi maishani mwangu?
Pengine jibu hapa linategemea maana ya wewe kusema “kung’ang’ana na dhambi!” Kama kwa kawaida wewe huwa unajisalimisha kutenda dhambi, basi kwa kweli Roho Mtakatifu hawezi kuwa anakuongoza. Lakini kama swali lako ni, “Je, nitakuwa nikitenda dhambi hata baada ya kujazwa Roho Mtakatifu?”—jibu hapo bila shaka ni “Ndio!” Mtu kujua wakati ametenda dhambi na yeye kushughulikia dhambi hiyo ni kitu ambacho kinajulikana kama “kupumua kiroho.”
Unaweza kujipata kwamba umetenda dhambi fulani na unalazimika kukiri mara kadha wa kadha kwa siku. Lakini huu sio udhaifu wa kiroho; hii ni ishara kwamba Roho Mtaktifu anafanya kazi maishani mwako! Kutambua dhambi maishani mwako na kuishughulikia ndilo jambo ambalo linajulikana kama “kupumua kiroho.”
Maana ya kupumua kiroho ni “kutoa pumzi”—kukubali dhambi yako kwa Bwana wakati umetenda dhambi. Unatambua kwamba umetenda dhambi na kwamba umechukua mahali pake Bwana kama kiongozi wa maisha yako. Kwa “kutoa pumzi” unaondoa mambo ambayo si safi maishani mwako, huku ukiomba msamaha wa dhambi, msamaha ambao ni haki yako kupitia kwa kifo chake Kristo msalabani.
Kupumua pumzi pia huhusisha “kuvuta pumzi”—kumwomba Mungu akujaze tena kwa Roho wake Mtakatifu, ya kwamba akuongoze tena. Kumbuka kwamba Yeye hakuachi eti kwa sababu umetenda dhambi. Lakini wewe umepuuza mwongozo wake, na sasa unataka tena kufuata uongozi wake. Umejifunza kumtumaini tena, jambo ambalo kwa kweli huchukua muda. Basi usife moyo unapojipata umeanguka dhambini: jifunze kujikokota, kuinuka, na kusimama tena.
Kitinda mimba wetu (mtoto wa mwisho kati ya watoto wetu watatu) alijifunza kutembea mwaka huu. Jambo hilo lilichukua muda. Yeye hakusimama tu alipofikisha mwaka mmoja na kuanza kwenda mbio. Hatua zake za kwanza zilikuwa za kuyumba-yumba hapa na pale. Mara nyingi yeye aliangukia vitu tofauti humo nyumbani. Lakini yeye kamwe hakukata tamaa. Mwishowe hatua zake zikaanza kupata nguvu, na akaanza kuwa na ujasiri wa kutembea. Lakini kwa kweli yeye angali huanguka wakati mwingine (na hata sisi wazazi wake!), lakini hata wakati kama huo yeye husimama tena na kuendelea kutembea.
Katika ulimwengu huu hakuna wakati utafika ambapo wewe hutaathiriwa na dhambi; maisha ambayo hayana dhambi hata moja hupatikana huko mbinguni. Tunavyoendelea kukua kiroho na kumjua Mungu zaidi ndivyo tutaendelea kukua katika uwezo wetu wa kuwa na mwelekeo wake Mungu katika mambo tunayokutana nayo, na ndiposa katika sehemu kadhaa maishani mwetu dhambi zetu zitapungua. Lakini hata ikifika wakati huo kungali kutakuwa na nyakati ambapo tutatenda dhambi na tutahitaji kupumua kiroho, iwe kwamba tutakuwa katika mwaka wa kwanza wa maisha yetu ya Kikristo, au hata katika mwaka wa saba.
3. Na je, ikiwa kwamba maisha yangu hayajabadilika sana?
Je, ushawahi kufikiri kwamba mahali ambapo umefika kwa sasa katika safari yako ya kiroho ni pale ambapo Mungu anataka uwe? Tayari tumesoma kuhusu Wakristo wa aina mbili, wa kimwili na wa kiroho. Lakini pia kuna kikundi kingine cha Wakristo: maanake Wakristo wapya. Kumbuka yale ambayo mtume Paulo aliwaambia Wakorintho? “Ndugu, mimi sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo.”
Miaka kadhaa kabla ya matamshi hayo, mtume Paulo alikuwa amewaongoza wengi wa waumini hao wa Korintho kumwamini Kristo. Wakati huo yeye hangewatarajia wawe Wakristo waliokomaa, wawe waumini wa kiroho. Lakini badala ya wao kukua kwa njia ya kawaida kama Wakristo, waumini hao wa Korintho walianza kuwa watu wa kimwili. Basi kama wewe ni Mkristo wa miezi kadhaa basi ungali Mkristo “mchanga”—sio Mkristo wa kimwili, bali Mkristo mchanga tu.
Katika kila mwezi wa Septemba, wakati mimi na familia yangu tulikuwa tukiishi sehemu ya katikati huko Magharibi ya Marekani, tulikuwa tukifanya ziara kutembelea mahali kuitwapo Bustani la Stova, mahali palipojulikana kama sehemu ya Mito Mitatu, huko Michigan. Sisi tulijua kwamba tukifika huko tutaweza kuona misururu ya miti ya tufaha, imepangwa vizuri laini. Hapo ndipo tulijaza vikapu vyetu kila aina ya matunda hayo.
Lakini katika sehemu ya nyuma ya shamba hilo kulikuwa na miti mingine ambayo haikuwa imejaa matunda ya tufaha. Kwa kweli miti hiyo haikuwa na matunda ya aina yoyote. Lakini miti yenyewe haikuwa miti iliyokufa; bali ilikuwa miti michanga tu. Mingine kati yao hata haikuwa imefika futi tano urefu. Hata ingawa miti ya miaka mingi ilikuwa imekomaa na kuinama kwa sababu ya kubeba matunda mengi, shughuli kubwa ya miti hiyo michanga ilikuwa ni kukua tu.
Basi kama wewe unamtii Kristo kwa sasa na kuamini kwamba nguvu zake zinakubadilisha, basi wewe upo mahali ambapo Mungu anataka uwe sasa. Usisumbuke sana eti kwa sababu huna “tunda.” Mimi sikuona moja ya miti hiyo michanga ikijifananisha na miti mizee. Kukua kama Mkristo ni jambo ambalo linaenda hatua kwa hatua, na kila hatua ni muhimu.
Ndiposa nimekuja kutambua kwamba ninapomtii Kristo na kukosa kujisumbua na kujilinganisha na Wakristo wengine, hapo ndipo mimi hupata furaha ya Ukristo wangu.