Unapoanguka (Dhambini)
Utafanya nini na dhambi??
Sikiliza makala hii:
Mamlaka ya ushuru ilipokea barua ifuatayo ambayo haikusema mwandishi ni nani:
Mabibi na Mabwana:
Hapa ndani kuna hundi ya dola 150 za Marekani. Mwaka jana nilifanya udanganyifu nilipokuwa nikijaza fomu zangu za ushuru, na kutoka wakati huo sijaweza kulala vizuri. Nikiendelea kupata shida ya kulala nitawatumia pesa zilizobaki za ushuru.1
Kila mmoja wetu hutaka kujihisi kuwa huru kutokana na maovu ambayo tayari tushafanya. Lakini swali ni: je, msamaha huo unatoka wapi?
Kama Mkristo, wewe umesamehewa dhambi zako zote. Pengine umesoma na kuamini hayo kutoka kwa Biblia. Lakini wajibu wako ni upi katika swala hili? Rafiki mmoja wangu ambaye anawapatia waumini wengi mawaidha anasema hivi: “Wakristo wengine huwa hawaamini kwa kweli kwamba wametenda dhambi; ilhali wengine huwa hawaamini kwamba wamekwisha samehewa.”
Lengo langu hapa ni kukusaidia kutambua ukweli wa dhambi, lakini pia utambue ukweli kuhusu msamaha unaotolewa na Kristo.
Dhambi Ni Nini?
Mwandishi Ernest Hermingway anasema kwamba, ukifanya jambo ambalo ni adilifu wewe baadaye utajihisi vizuri; lakini kama jambo hilo sio adilifu baadaye utajihisi vibaya. Haya ni maoni ambayo yanapendwa na watu wengi – na wengi wanaishi kwa kanuni hiyo. Lakini maoni hayo hayalingani na biblia. Kulingana na biblia dhambi ni mtu kutaka kwenda kwa njia zake mwenyewe, badala ya kwenda kwa njia zake Mungu.
Je, Mungu anachukulia dhambi vipi? Kamwe Yeye hawezi kuivumilia dhambi. “Wewe ni mtakatifu kabisa, huwezi kutazama uovu, huwezi kustahimili kamwe kuona mabaya” (Habakuki 1:13a). “Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake” (1 Yohana 1:5a).
Huenda jambo hili lisionekana kuwa muhimu. Si ni kweli kwamba Yesu alilipa gharama yote ya dhambi zetu? Kwa nini sisi tujishughulishe na dhambi ilhali Mungu anatupenda na ametupatia mpango kabambe kwa maisha yetu? Wengine wanasema tunahitaji kuchukua dhambi kuwa makosa tu, makosa kidogo kidogo ya hapa na pale.
Lakini mwelekeo wa Mungu kuhusu dhambi hauko hivyo. Kwa ajili ya dhambi moja tu Adamu na Hawa walifukuzwa kutoka paradiso. Na kwa sababu ya dhambi Mungu alileta gharika kwa watu wote duniani katika siku za Noa. Yeye pia alichoma miji ya Sodomu na Gomora kwa sababu ya upotovu wao. Dhambi pia iliwadumisha wana wa Israeli jangwani kwa miaka arobanne.
Mungu anachukia dhambi. Lakini sisi huhisi dhambi kuwa ni kitu kizuri, na kuitenda kila mara. Kama Adamu na Hawa, sisi hudhani kwamba tunaweza kujua uovu na kuweza kushinda uovu huo pia. Lakini kwa kweli hatufanyiki kuwa kama Mungu kwa kutenda dhambi. Mungu mwenyewe anajua kwamba kuna uovu, lakini Yeye si mwovu, na kamwe Yeye hajisalimishi kwa uovu. Lakini sisi huvutiwa na uovu, na wakati mwingi tunajisalimisha kwa uovu huo.
Mwenye Makosa
Unapotenda dhambi Roho wa Mungu ambaye yuko ndani yako anahuzunika. Wakati mwingine Yeye atakufanya ujisikie kuwa na makosa. Wakati unatenda dhambi wewe huwa umechagua kuishi nje ya mapenzi yake Mungu. Jambo hili halimfanyi Mungu kukuchukia. Yeye angali anakupenda. Lakini hili ni jambo ambalo humletea huzuni: “Msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, maana Roho huyo ni alama ya Mungu kwenu kwamba nyinyi ni watu wake, na thibitisho kwamba siku itakuja ambapo Mungu atawakomboeni” (Waefeso 4:30). Ili uweze kuelewa vile ambavyo dhambi inakudhuru hebu tutazame tofauti kati ya uhusiano wako na Mungu ukilinganishwa na ushirika wako na Mungu.
Uhusiano Wako na Mungu | Ushirika Wako na Mungu |
Ulianza wakati wewe ulimpokea Kristo (Yohana 1:12) | Ulianza wakati ulimpokea Kristo (Wakolosai 2:6) |
Ni wa milele (1 Peter 1:3,4) | Unaweza kuwa na kizuizi (Zaburi 32:3-5) |
Mungu pekee ndiye huudumisha (Yohana 10:27-29) | Kwa upande moja wewe ndiwe ambaye huudumisha (1 Yohana 1:9) |
Haubadiliki (Waebrania 13:5) | Hubadilika wakati umetenda dhambi (Zaburi 66:18) |
Dhambi yenyewe haidhuru uhusiano huo wako wa milele na Mungu — jambo ambalo lilitatuliwa wakati ulimwamini Kristo kuwa alilipa gharama ya dhambi zako. Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zako zote – za kale, za sasa, na hata za siku zijazo. Wakati Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zako, maisha yako yote yalikuwa yangali ni ya baadaye. Kwa sababu ya imani yako kwa Yesu wewe umesamehewa dhambi zako kabisa. Uhusiano wako na Mungu uko timamu.
Lakini dhambi inadhuru ushirika wako na Mungu. (Maana ya ushirika ni uhusiano wako wa kila siku na Mungu hapa duniani). Dhambi inadhuru mawasiliano kati yako na Yeye na utumishi wako kwa mapenzi yake. Dhambi inakukosesha umakini katika mambo ambayo Kristo angetaka uyawaze na kuyatenda.
Zaburi 32:3-5 inasema: “Wakati nilipokuwa sijakiri dhambi yangu, nilikuwa nimedhoofika kwa kulia mchana kutwa. Mchana na usiku mkono wako ulinilemea; nikafyonzwa nguvu zangu, kama maji wakati wa kiangazi. Kisha nilikiri makosa yangu kwako; wala sikuuficha uovu wangu. Nilisema ninakuungamia makosa yangu ee Mwenyezi-Mungu, ndipo nawe ukanisamehe dhambi zangu zote.”
Huu ndio mwelekeo ambao unafaa kuhusu dhambi. Mwanazaburi hakujaribu kukana dhambi yake. Pia akili zake hazikutekwa nyara na dhambi hiyo. Badala yake yeye aliungama dhambi yake.
Kuungama na Kutubu Dhambi
Maana ya kuungama na kutubu dhambi ni nini? Kwanza kabisa maana ya kuungama ni kukubaliana na Mungu. Yeye tayari ashajua kwamba wewe umetenda dhambi, kwa hivyo ni bora zaidi wewe kuwa mkweli kwa swala hilo! “Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote” (1 Yohana 1:9). Maana ya kuungama ni sisi kukiri dhambi zetu kwa hiari, na kukubali kwamba Mungu amechukizwa kutokana na dhambi yetu. Kuungama sio kumshawishi Mungu kukupatia msamaha. Kristo tayari ashalipa gharama ya dhambi zetu zote, na msamaha wa Mungu hupatikana papo hapo wakati tumeungama dhambi zetu. Sababu ya Mungu kuweza kukupatia msamaha ni kutokana na kifo cha Yesu msalabani, na sio kutokana na nguvu za unyenyekevu wako, ambao wewe umedhihirisha unapoungama dhambi zako. Nayo maana ya kutubu ni mtu kubadilisha mienendo yake kwa dhambi ambayo ametenda. Msamaha unahusisha kukubaliana na Mungu kwamba wewe ulifanya makosa, na kwamba hutaki kuendelea kufanya dhambi hiyo.
Lakini Mimi Ningali Najihisi Kuwa na Hatia!
Kuna wakati ambapo utaendelea kuhisi kwamba ungali na hatia hata baada ya kuungama dhambi zako. Wakati mwingi sisi hujihisi kwamba tunakuwa wa kiroho zaidi kwa kujishusha hadhi yetu kutokana na dhambi tuliyotenda; tunajihisi kwamba tukiweza kujishusha Mungu atafurahishwa na unyenyekevu wetu.
Lakini Mungu mwenyewe hatuoni hivyo. Sehemu moja ya kuungama dhambi zetu ni kumshukuru Mungu kwa sababu tayari dhambi zetu zote zishalipiwa na Kristo. Ndiposa kutokana na hayo Mungu anasema, “Nitawasamehe makosa yao, wala sitakumbuka tena dhambi zao” (Waebrania 8:12). Kutoa shukrani ni jambo linalotokana na imani, kwa sababu wewe unatenda kulingana na yale ambayo Mungu amesema kukuhusu wewe mwenyewe na kuhusu dhambi yako; badala ya wewe kutenda kulingana na vile unavyojihisi. Tendo la kujishusha hadhi kwa sababu ya dhambi yako ni jambo linaloletwa na mtu kuweka fikra katika dhambi yake badala ya kuwaza kuhusu msamaha ambao anapewa na Kristo.
Wakati mwingine sisi hufanya makosa ya kuchukulia majaribu kuwa ni dhambi. Lakini hebu kumbuka kwamba kila mtu hujaribiwa. Hata Yesu mwenyewe alijaribiwa . . . lakini Yeye kamwe hakujisalimisha kwa majaribu hayo – kamwe hakutenda dhambi. Kama basi wewe unajaribiwa usianze kujilaumu. Badala yake unaweza kuchagua kuachana na mawazo hayo yanayoleta majaribu na kumwomba Mungu akupatie nguvu za kuepuka dhambi. Basi usijihisi makosa kutokana na kujaribiwa. Aya moja ya Biblia ambayo mtu anaweza kukumbuka anapojaribiwa ni 1 Wakorintho 10:13.
Mungu amekusamehe maovu yote ambayo umetenda. “Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo” (Warumi 8:1). Yeye hatazami nyuma kuona dhambi zako au makosa yako kwa mtazamo wa hukumu, na wewe unahitaji kufuata mfano huo wake. Zaidi ya yote Mungu amesema, “Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu” (Waebrania 10:17). Wingu la lawama na hatia limeondoka! Hebu basi kubali msamaha kamili wa Mungu.
“Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo” (Warumi 8:2). Maisha ya Ukristo ni maisha ya uhuru: uhuru kutokana na hatia, na uhuru wa kuishi kulingana na vile Mungu anavyotaka, na ni maisha ambayo humtosheleza mtu sana. Safari ya Kikristo ni ya mtu kukua, kufanyika kuwa kama Kristo, na kumwangazia Kristo maishani mwake. Lakini kukua kwenyewe huchukua muda!
(1) Mwandishi Charles Swindoll, Come Before Winter (Fika Kabla ya Msimu wa Baridi) Portland, OR: Multnomah Press, 1985, ukurasa 89.